Article Preview

Usimilishaji wa Vipengele vya Maandishi ya Kale: Mfano wa Tenzi za Fumo Liyongo na Mwana Kupona

Abstract: Tenzi za kale za Kiswahili kama Fumo Liyongo na Mwana Kupona ni hazina kubwa ya urithi wa kifasihi, historia na utamaduni wa Waswahili. Hata hivyo, tenzi hizi ziliundwa kwa hadhira ya watu wazima na zimejaa lugha ya kale, mafumbo, mitindo ya kishairi tata pamoja na maudhui mazito ya kifalsafa na kidini ambayo watoto hawawezi kuyafikia kwa urahisi. Hali hii inaleta changamoto ya jinsi urithi huu muhimu unaweza kuwasilishwa kwa watoto bila kupoteza maana yake ya asili. Kwa hiyo, utafiti huu unalenga kuchunguza namna ambavyo vipengele vya msingi vya tenzi za kale vimebadilishwa kupitia usimilisho ili kulenga hadhira ya watoto bila kupoteza utambulisho wa kihistoria na kitamaduni wa Waswahili. Wasanii wa kisasa wamefanya jitihada za kusimilisha tenzi hizo kwa kuzibsahilisha kuwa fasihi ya watoto. Hata hivyo, tafiti za kina kuhusu jinsi masimilisho haya yamesahilishwa na athari zake katika uwasilishaji wa historia, utamaduni na maadili kwa watoto bado ni chache. Makala hii inachunguza ukarabati wa vipengee katika tenzi za kale ili kulenga hadhira ya watoto, kwa kuzingatia mifano ya Utenzi wa Fumo Liyongo (UwFL) na Utenzi wa Mwana Kupona (UwMK). Data ya utafiti ilikusanywa kupitia usomaji wa makini wa matini chasili mathalan; UwFL na UwMK pamoja na matini lengwa; Kisa cha Fumo Liyongo (KcFL), Wasifu wa Mwana Kupona (WwMK) na Mkasa wa Shujaa Liyongo (MwSHL). Uchambuzi ulifanywa kwa misingi ya Nadharia ya Usimilisho ya Hutcheon (2013). Ukarabati uliobainika kutokana na utafiti huu ni pamoja na: urahisishaji wa lugha ya Kiswahili cha kale kwa kutumia Kiswahili sanifu na sentensi fupi; kupunguzwa kwa maudhui magumu ya kidini na kuelekezwa katika mafunzo ya maadili; kuongeza wahusika na kuwapa tabia zinazolingana na ulimwengu wa watoto; kubadilisha muundo wa kishairi kuwa nathari na mashairi mepesi; kugawanya simulizi katika sura fupi na kuongeza michoro inayosaidia uelewa wa watoto. Vilevile, mandhari na miji ya kihistoria kama Lamu na Pate iliwasilishwa kwa namna inayodumisha utambulisho wa Kiswahili. Kutokana na hitimisho kwamba usimilisho umesababisha urahisishaji wa lugha na kupunguzwa kwa maudhui mazito ya kifalsafa, hali iliyoacha watoto na ufahamu mdogo wa utajiri wa ushairi wa kale, utafiti unapendekeza kuwa mashirika ya kijamii na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) yashirikiane na shule ili kuunda vipindi vya kusoma ambapo tenzi asilia na kazi zilizosimilishwa zitaweza kufundishwa kwa pamoja ili kuimarisha ujifunzaji wa watoto. 

Maneno makuu: Fasihi ya Watoto, Hadhira ya Watoto, Matini,Ttenzi za Kale, Usimilisho, Vipengee 

Information

All rights reserved © IJSDC.org 2025